Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ambaye alikuwa anatamani kabla ya
kumaliza muda wake wa urais kufanikisha zoezi la kupatikana kwa katiba
mpya nchini. Picha na Maktaba
Kwa ufupi
Profesa Mpangala ni miongoni mwa Watanzania
waliozungumzia uamuzi wa kumaliza Bunge la Katiba Oktoba 4, mwaka huu
badala ya Oktoba 31, huku upigaji kura ukisogezwa mbele hadi baada ya
Uchaguzi Mkuu 2015, wakibainisha kuwa kitendo hicho ni matokeo ya ubabe
wa wanasiasa wa kutotaka kukubali ushauri, licha ya kuelezwa kasoro za
mchakato mzima tangu awali.
Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Gaudence
Mpangala amesema matatizo yanayolikumba Bunge Maalumu la Katiba
yamezungumzwa na watu wengi na sasa yamegeuka wimbo wa Taifa, lakini la
muhimu ni maridhiano.
Profesa Mpangala ni miongoni mwa Watanzania
waliozungumzia uamuzi wa kumaliza Bunge la Katiba Oktoba 4, mwaka huu
badala ya Oktoba 31, huku upigaji kura ukisogezwa mbele hadi baada ya
Uchaguzi Mkuu 2015, wakibainisha kuwa kitendo hicho ni matokeo ya ubabe
wa wanasiasa wa kutotaka kukubali ushauri, licha ya kuelezwa kasoro za
mchakato mzima tangu awali.
Profesa Mpangala alisema, “Nilifanya utafiti na maprofesa
wenzangu wawili na kuja na mapendekezo ya kusitishwa kwa Bunge hili
lakini hakuna aliyetaka kusikiliza.”
Alisema kuwa hata fedha zilizotengwa sasa
zimetumika bure na hata hiyo 2016 hakuna kitakachoendelea kama pande
mbili zinazovutana hazitakubaliana katika mambo ya msingi. Wakili na
kiongozi mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Harold Sungusia alisema tangu mwanzo kulikuwa na vitu vitatu
vilivyoonyesha wazi kuwa mchakato huo haukulenga kuwapatia Watanzania
Katiba Mpya.
Sungusia alitaja vitu hivyo kuwa ni suala la
Katiba Mpya kutokuwa katika Ilani ya CCM... “Kilikuwa kitu kipya na
lilikuwa wazo la Rais Jakaya Kikwete. Kumbuka mwanzoni CCM haohao
walisema hakuna haja ya kuandika Katiba na ndiyo haohao wako bungeni
wakibadilisha Rasimu watakavyo.
“Pili, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa na kasoro nyingi.
Sheria hii iliandaliwa kwa ajili ya kutopata Katiba Mpya. Walibadilisha
Kifungu cha 36 na kukiweka katika sheria ya kura ya maoni ambayo sasa
inaeleza kuwa iwapo watakaopiga kura hawatazidi nusu kwa mara mbili,
unaanza mchakato upya.”
Alisema kasoro ya tatu ni kuchanganya majukumu ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba na kusisitiza
kuwa hakukuwa na ulazima wa kuwapo na vyombo hivyo viwili kwa wakati
mmoja kwa kuwa kimoja tu kingetosha kutengeneza rasimu.
Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia (Azaki), Irenei
Kiria alisema, “Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ilitakiwa kupelekwa katika kura ya maoni moja kwa moja, kitendo cha
kuipeleka bungeni ilikuwa ni kupoteza muda.”
Kiria alisema hata utungaji wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ulikuwa na tatizo kutokana na kuruhusu wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Tangu mwanzo hakukuwa na nia ya kupata Katiba
Mpya. Bunge hili lilitakiwa kuahirishwa tangu siku ambayo Rais Kikwete
alitoa hotuba yake ya kufungua Bunge hilo maana alionyesha wazi kuwa CCM
haitaki Katiba Mpya.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni