Jumatano, 18 Februari 2015

WALIOMTEKA ALBINO GEITA WAUNDIWA KIKOSI KAZI

 NA ELIUD DALEI,GEITA 17/02/2015

JESHI la polisi Mkoa wa Geita imeunda kikosi maalum kwa ajili ya kuwasaka na kuhakikisha linawakamata watu wasiojulikana waliompora mikononi mwa mama yake na kuondoka naye mtoto Yohana Bahati mwenye ulemavu wa ngozi(ALBINO)mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita. Tukio hilo la kuporwa mtoto Bahati,na linalohusishwa na imani za kishirikina hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa udiwani,ubunge na Urais limetokea feb 15 saa 2 usiku katika kitongoji cha Ilyamchele,kijiji cha Ilelema wilayani Chato mkoani Geita,huku watekaji wakimjeruhi kwa mapanga mama wa mtoto huyo.





 Akizungumza na wanahabari ofisini kwake,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Joseph Konyo amesema kikosi kazi hicho kitazunguka ndani na nje ya Wilaya za Mkoa wa Geita kikishirikiana na Polisi wa Mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa. Kamanda Konyo alisema lengo la operesheni hiyo maalum ni kuwasaka watu hao na pia kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya walemavu katika juhudi za kukomesha matukio hayo, ambayo yameelezwa kuanza kuibuka tena Mkoani kwake.

 ‘’Tayari Operesheni hiyo maalum imeanza ninawaomba wananchi wa Mkoa wa Geita ni ile ya Jirani kutoa taarifa kwenye vyombo husika pale inapokuwa na mashaka na mtu Fulani na si kuwapa ushirikiano watu hao kwani ukarimu mwingine ni wa kipumbavu mtu humjui unamuonyesha hadi njia ya kupita kwa namna hii hatuwezi kukomesha vitendo hivi lazima ifike mahali wananchi tuamke’’alisema Konyo. Kuhusu wapiga ramli Kamanda konyo alisema jeshi la Polisi limeshatoa maelekezo kwa viongozi wa waganga wa jadi na tayari operesheni maalum kuwatafuta na kuwashika wapiga ramli Mkoani hapo na kuwashtaki ilikwishaanza kufanyika.

Huku akiongeza kuwa wapiga ramli hao wanajulikana na wananchi hivyo anawaomba wananchi kusaidia kwa kushirikiana na viongozi hao wa waganga kuwatambua. Mbali na hayo, Konyo ameyataka madhehebu ya dini mbalimbali na mashirika ya kijamii kutoa elimu juu ya jambo hilo. Huku sababu kubwa iliyotajwa inayosababisha watu kutafuta viungo hivyo vya binadamu inaelezwa kuwa ni kupata utajiri na kutoa mikosi kwa wanasiasa wanaosaka nafasi mbalimbali za uongozi kwenye jamii.

 Awali ilielezwa kuwa,watu wanaodaiwa kufanya unyama huo walikuwa wawili ambao walivamia nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo wakiwa na mapanga na kisha kutoweka naye kusikojulikana baada ya kuwazidi nguvu wazazi wake. Kwa mujibu kamanda wa polisi mkoani Geita,Joseph Konyo,alisema tukio hilo limetokea saa 2 usiku wakati mama wa mtoto huyo,Ester Jonasi(30)wakati akiwa katika harakati za kuandaa chakula cha usiku.

Alisema watu hao wakiwa na mapanga baada ya kufika katika familia hiyo,wamteka mama yake na katika kunyang'anyana walilazimika kutumia mapanga kwa kumjeruhi mama wa mtoto huo. Aliongeza kuwa,Familia hiyo inawatoto watatu wote Albino ambapo wakati mtoto mwingine anatekwa kaka yake alikuwa kwa jirani anacheza na aliporejea nyumbani alikuta tukio limetokea. Konyo alisema pamoja na juhudi za wananchi na polisi kufika eneo la tukio hazikuzaa matunda kuwakamata watu hao na kwamba juhudi za kuwatafuta watuhumiwa hao zinaendelea na hivyo kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kuwasaka watu hao.

"Tukio ambalo ni la kwanza katika mkoa wetu wa Geita..limetuweka katika mazingira magumu sana.lakini tumejipanga timu ya makachero inaendelea kuchunguza na kwamba tutahakikisha huyu huyo mtoto anarudi" Tayari baba wa mtoto huyo,Bahati Msalaba anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi Hili ni tukio la pili kutokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili ambapo Disemba 27,mwaka jana mtoto Pendo Emanule(4)wa Ndami Misungwi alitekwa na watu wasiojulika na hadi sasa bado hajapatikana wala watekaji wa mtoto huyo hawajakamatwa.

Mwisho. .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni