Alhamisi, 26 Juni 2014

walia na jaji mkuu

WALIA NA JAJI MKUU: Mahabusu 10 wavua nguo Nyankumbu leo kupinga kesi zao kuchelewa, wataka kuwaona AG F. Werema, Jaji Mkuu O. Chande na RC wa Geita S. Magalula.

Na Eliud Dalei,Geita 26/06/2014
Matukio ya ajabu yanayofanywa na mahabusu wanaoshinikiza kesi zao kusikilizwa haraka ikiwa ni mbinu wanazoamini zitasaidia katika kile wanachoeleza kuwa ni kudai haki zao yanaendelea kuonekana ambapo jana mahabusu Wilayani Geita walifanya tukio la aina yake.
Mahabusu wanane  wanaoshikiliwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za mauaji jana wakati wakitoka mahakamani baada ya mashauri yao kuahirishwa waliung’ang’ania mlingoti wa bendera ya Taifa huku wote wakivua nguo zote na kubaki mtupu.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3:15 hadi saa 4:15 asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Geita.
Mahabusu hao hao walivua nguo zote na kubaki mtupu na kisha kupiga kelele wakiwa wameshikilia mlingoti waakieleza kilio chao.
“Haiwezekani tangu mwaka jana tulipokamatwa hadi sasa kesi zetu zinapigwa kalenda. Wengine tumebambikiwa kesi. Tunaomba haki zetu, polisi wanatuonea, vyombo vya habari tunaomba mtusaidie tumekaa muda mrefu bila kusikilizwa na hatujui hatma yetu tangu mwaka 203,tulipokamatwa. Tumechoka kukaa mahabusu, tunaomba kesi zetu zisikilizwe.” Alisema Iliza Warioba mmoja wa mahabusu hao.
Waliovua nguo na kung'ang'ania mlingoti,nje ya mahakama ya Mwanzo nyankumbu ambayo kwa sasa inatumika kama ya wilaya baada ya ile ya wilaya kutumika kama mahakama kuu ni pamoja na Iliza Warioba,Stephen James,Kalebu Ochieng na Masha Joseph.
Wengine ni Omari Juma,Nicholaus Kisinza,Daud Lumumba,Gofrey Luta,Emanuel Daud na Saimon Panya.
Mkuu wa polisi wa wilaya ya Geita,Busee Bwire aliwataka watuhumiwa hao waondoke katika mlingoti na kuvaa nguo ili waingie kwenye gari ili warudishwe gerezani kwani kitendo walichokuwa wakikkifanya ni kosa la jinai lakini waligoma..
“Pamoja na maamuzi yenu haya, lakini mtambue mnavunja sheria na hili ni kosa jingine la jinai, hivyo ni vyema mkaondoka kwenye mlingoti huu na kuingia kwenye gari Malalamiko yenu tumeyasikia na yatashughulikiwa.” Alisema Bwire
Hali hiyo,ilimlazimu Ocd Bwire kuagiza askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU na walipofika eneo hilo la mahakama walitaka kuwatoa kwa nguvu kwenye mlinoti mahabusu hao ambao walitishia kushusha bendera hiyo ya taifa iwapo askari yeyote angewagusa.
''Tulishakufa tayari tukiwa gerezani hivyo askari atakayetugusa hapa tuko tayari kufa naye,tumeshachoka na ndiyo maana hapa tumeishika serikali(mlingoti)tuanomba mtuache au aje mkuu wa mkoa na mwanasheria wa serikali achukuwe kero zetu''walisikika mahabusu hao wakichimba mkwara.
Kufuatia hali hiyo,Katibu tawala wa Wilaya ya Geita,Gasto Gaspari alifika eneo hilo akidai ameagizwa na mkuu wa mkoa huo kuja kuwasikiliza malalamiko yao ambapo walimueleza kila kitu na kuahidi kufikisha kilio chao kwa seriakaali.
Baadaye alikuja mwanashheria wa serikali Hezron Mwasimba aliyewasihi wakubali kupanda kwenye gari na kurudishwa gerezani huku akiwahakikishia majira ya saa saba jopo la wanasheria,wakiwemo mahakimu na viongozi wa serikali kufika lilipo gereza hilo kwa ajili ya kuzungumza na mahabusu wote wa gereza hilo.
Kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa mahabusu wakilalamikia kesi zao kuchukua muda mrefu na hata wanaponyoosha mikono kuwaeleza mahakimu wamekuwa wakidai kutosikilizwa.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni