BAKORA ZATEMBEA MSIBA WA MAMA WA MWANDISHI WA HABARI
Ni baada ya wajukuu kung’ang’ania ndani ya kaburi wakitaka
mlungula
Baba Paroko atimua mbio,aita polisi kuokoa jahazi
Mazishi yafanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi
Na Eliud Dalei,Sengerema
06/10/2014
WAJUKUU wa marehemu Sabina Ngalu(77),ambaye ni mama wa mwandishi
wa habari wa kujitegemea Salum Maige anayeandikia magazeti ya Mwananchi,The Citizen na Radio
Free Africa(RFA) ya jijini Mwanza wamejikuta wakicharazwa bakora eneo la
makaburi muda mfupi kabla ya mazishi.
Tukio hilo la aina yake limetokea mwishoni mwa wiki
iliyopita saa 5 asubuhi katika Kitongoji cha Nyamwanza kata ya Sima Wilayani
Sengerema Mkoa wa Mwanza muda mfupi baada ya mwili wa marehemu kuwasili eneo la
mazishi kwenye shamba lake ukitokea kanisa la Roman Catholic Parokia ya Yesu
Kirsto Mfalme la mjini Sengerema.
Chanzo cha wajukuu
hao zaidi ya 10 kuchacharazwa bakora ni utovu wa nidhamu waliouonyesha wa kung’ang’ania
ndani ya kaburi lililokuwa limeandaliwa rasmi kwa ajili ya kuuhifadhi mwili wa
marehemu Ngalu(77).
Sababu za wajukuu hao kung’ang’ania ndani ya kaburi hilo
walitaka wapewe Ng’ombe mmoja au pesa taslimu Tshs 100,000,kwa mjibu wa mila na
desturi za kabila la Kisukuma jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya wanandugu
waliodai mila hizo zilikwishapitwa na wakati na kuwataka watoke kaburini ili
taratibu za mazishi ziendelee.
Baadhi ya wajukuu walioonja joto la jiwe ni pamoja na Andrea
Mabula,Sabina Bukuru,Johari Bukuru,Asha Bukuru,Faida Bukuru,Yuves Petro,Semen
pamoja na koiongozi wao Enos Ntilaga.
Hata hivyo wajukuu hao waligoma kutoka ndani ya kaburi hilo
huku wakisisitiza kuwa wapo tayari kufa lakini si kutoka ndani ya kaburi hilo
bila kupatiwa ng’ombe mmoja au kiasi hicho cha pesa.
Kitendo cha wajukuu hao kugoma kutoka ndani ya kaburi hilo,kilimchefua
Padre Nicodemus Mayala ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mfalme Sengerema
Mwanza ambaye aliamua kuondoka eneo la maziko huku akitaarifu polisi kuhusiana
na vurugu hizo.
Kufuatia hali hiyo,kaka wa marehemu Enosi Ngalu,aliyeonekana
kukerwa na kitendo hicho alitafuta mkwaju(fimbo) ndefu kisha kutinga eneo
lilipochimbwa kaburi hilo na kuanza kutembeza mkong’oto wa nguvu kwa wajukuu
hao waliokuwa ndani ya kaburi hilo.
Kitendo ambacho kilizidisha hasira kwa wajukuu hao ambao
wakiwa ndani ya kaburi walianza kujibu mapigo kwa kumrushia mchanga mjomba wao
huyo ambaye alizidiwa ujanja na kuamua kusitisha zoezi lake la kutembeza bakora
mithili ya katuni maalufu yam zee kifimbo cheza wa gazeti la Sani na kutimua
mbio.
WAOMBOLEZAJI WAKUBALI YAISHE
Kufuatia hali hiyo,mmoja wa waombolezaji aliamua kukubali
yaishe baada ya kuona wajukuu hao walikuwa hawabipu kisha kuzama mfukoni na
kutoa kiasi cha pesa walichohitaji wajukuu hao na kuwapa na ndipo walipokubali
kutoka ndani ya kaburi hilo ili mazishi yaendelee.
PADRE AGOMA KUONGOZA IBAADA YA MAZISHI.
Ili kuonyesha alikerwa na kitendo hicho,Padre Mayara ambaye
kwa wakati huo alikuwa amewekwa kitimoto na baadhi ya wanandugu wakimsihi
kutosusia mazishi hayo mita 200 kutoka eneo la kaburi aligoma kurejea kaburini
kuongoza ibada ya mazishi hayo.
‘’Hata kama wameshatoka ndani ya kaburi mie siwezi kurudi
tena huko kuongoza ibada ya mazishi maana hili jambo limefanywa kinyume na
taratibu za sisi wakristo maana haya ni mambo ya kipagani yalipaswa yafanywe
kipagani’’alisikika Padre Mayala akitia ngumu.
BABA WA WATOTO AZIDI KUMWANGUKIA PADRE
‘’Ni kweli hili limeshafanyika tunaomba utusamehe baba
paroko na sisi kama wazazi tunajua jinsi ya kuwawajibisha hawa watoto hawawezi
kutushinda,cha msingi hapa ni wewe kusamehe hili lililotokea turudi kaburini ukaongoze
misa ya mazishi tumsitili ndugu yetu maana saaa 2 zimepita jeneza linapigwa jua
tunakuwa hatumtendei haki marehemu ambaye anapaswa kupumzika’’alisikika mmoja
wa wanafamilia ya marehemu akimshauri Padre bila mafanikio.
PADRE ALEGEZA MASHARTI
Baada ya vuta nikuvute hatimaye Padre Mayala aliwataka wajukuu
hao kurudisha pesa waliyochukua na
kuwataka radhi wanamtaa huo na ndipo anaweza kurudi eneo la kaburi kuongoza
ibada ya mazishi kinyume na hivyo alisisitiza asingeweza kufanya hivyo kwani
kitendo hicho kimekiuka misingi ya dini nyao.
WAJUKUU WAKUBALI KWA SHINGO UPANDE KURUDISHA PESA
Kutokana na hali hiyo wajukuu hao waliitwa mbele ya Padre na
mbele ya wanamtaa huo kisha waliomba samahani ikiwa ni pamoja na kurudisha pesa
hiyo kwa aliyekuwa ameitoa na ndipo Padre aliporejea eneo la kaburi na kuongoza
ibada ya mazishi.
POLISI WATINGA MAKABURINI
Majira ya saa 6:30 polisi zaidi ya wane kutoka kituo cha
Sengerema wakiwa na bunduki aina ya SMG,na zile za mabomu ya machozi walifika
eneo hilo kufuatia simu iliyokuwa imepigwa na Padre Mayala wakati vurugu hizo
zikiwa zimepamba moto.
Baada ya polisi kufika eneo hilo walimkuta Padre Mayala
akiendelea na ibada ya mazishi na wao wakaweka kambi kwa muda huku
wakizungukazunguka eneo hilo na baadaye waliondoka baada ya kuona hali iko
shwari eneo la mazishi.
TIMBWILI LAHAMIA NYUMBANI KWA MAREHEMU
Majira ya saa 7:15 baadaa ya kutoka makaburini wajukuu wale
waliwahi nyumbani kwa marehemu Mtaa wa
Mlimani Kata ya Nyatukala Wilayani Sengerema kisha kuanzisha timbwili jingine
kwa kuficha chakula na vyombo vya kupakulia wakidai warudishiwe pesa yao
waliyokuwa wameirejesha makaburini kwa shinikizo la baba paroko.
‘’Leo hali mtu hapa,mmetucharaza bakora na pesa yetu
mkatunyang’anya sasa tuko tayari kupigwa mpaka mtuuwe lakini chakula hakitoki
hapa au la sivyo mturudishie pesa yetu’’alisikika Enos Ntilaga mjukuu wa
marehemu akichimba biti huku akiwa anahamisha masufuria ya chakula kwa
kushirikiana na wenzake na kwenda kuyaficha.
MMOJA WA WAOMBOLEZAJI AOKOA JAHAZI
Baada ya timbwili hilo kukolea kama moto kwenye majani makavu,mmoja wa wafiwa
alizama mfukoni kisha kutoa kiasi cha fedha kilichotakiwa na kuwakabidhi wajukuu
hao ambao walirudisha chakula jikoni na taratibu za ndugu za jamaa na marafiki
wa wafiwa kupata chakula ziliendelea huku baadhi ya wafiwa wakiwa tayari
wameamua kuondoka na kwenda kutafuta chakula mahotelini akiwemo Maige ambaye ni
mtoto wa marehemu na waandishi wengine wa habari waliofika kumlaki likiwemo0
gazreti hili .
YABAINIKA WENGINE WALIKUWA WAJUKUU FEKI
Mtoto wa marehemu, Maige ambaye ni mwandishi wa habari
akizungumzia tukio hilo alidai kuwa,si wote walioanzisha timbwili hilo ni
wajukuu wa marehemu mama yake bali na vijana wa kihuni waliingilia sakata hilo.
‘’Kama huyo unayemuona pale(huku akimuonyesha mwandishi wa
habari)si mwanafamilia wala si mjukuu wa marehemu mama ni mhuni tu na sijui hata
alikotokea naona atakuwa mzamiaji wa chakula’’alisema Maige kwa masikitiko.
KAKA WA MAREHEMU AAHIDI KUWASHUGHULIKIA
Kwa upande wake kaka wa marehemu aliyewacharaza bakora
wajukuu hao,alidai kuwa wanasubilia siku arobaini ziishe waitishe kikao cha ukoo
kwa lengo la kuwawajibisha wale wote waliozua tafrani msibani.
MWENYEKITI WA ENEO APIGWA BUTWAA
Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mlimani aliyekuwa eneo hilo,Joseph
Numbuyamwana alishangazwa na hatua hiyo huku akiwasihi wale wote wanaokusudia
kufanya vitendo hivyo nyuma ya pazia la kimila wafanye kwa kuangalifu kuepuka
kuwakwaza viongozi wa dini kama ilivyotokea kwenye msiba huo.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni