Jumatano, 18 Februari 2015

MWILI WA ALBINO WAPATIKANA HAUNA VIUNGO

 NA ELIUD DALEI,GEITA 18/02/2015

HATIMAYE baada ya makachero wa Polisi Mkoani Geita wakishirikiana na wananchi wa kitongoji cha Mapinduzi katika Kijiji cha Lumasa jirani na Hifadhi ya Biharamlo Kagera wamefanikiwa kuupata mwili wa Mtoto Yohana Bahati(mwaka mmoja na miezi sita)ukiwa umekatwa miguu na mikono huku huzuni ikitanda eneo hilo.




Mwili wa mtoto Bahati ambaye ni mlemavu wa ngozi(Albino) huku akiwa amekufa uliokotwa Feb 17 saa 12 jioni na wakazi wa eneo hilo waliokuwa doria tangu mtoto huyo alipoporwa mikononi mwa mama yake,Feb 15 mwaka huu kwenye hifadhi yam situ wa Biharamlo Kagera.

 Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita Joseph Konyo alilieleza Gazeti hili kuwa mwili huo uliokotwa kwenye shamba la mahindi lililopo katika hifadhi ya Biharamlo Kagera. Kwa mjibu wa Kamanda Konyo,mwili huo uliokotwa kwa jitihada za wakazi wa Kitongoji cha Mapinduzi Kijiji cha Lumasa Wilayani Chato Mkoani Geita waliokuwa doria wakishirikiana na makachero wa Jeshi la polisi waliomwagwa huko kwa ajili ya msako wa watu waliohusika na unyama huo.

 Kamanda Konyo aliongeza kuwa baada ya mwili huo kuokotwa ulichukuliwa na kwenda kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya wilaya ya Chato kusubiri uchunguzi na taratibu za mazishi.

‘’Ufuatiliaji wa tukio hilo la mtoto Bahati ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyeibwa Feb 15 saa 2 usiku umefanyika kwa nguvu ya wananchi na polisi na jana saa 12 jioni tumempata akiwa ameuawa huku amekatwa viungo vyake miguu na mikono yake yote’’

‘’Mwili huo tumeukuta umetelekezwa kwenye shamba la mahindi lililopo kwenye hifadhi ya yam situ wa Biharamlo Kagera na tumeuchukua na kuuhifadhi kwenye hospitali ya Wilaya ya Chato ukisubili uchunguzi na taratibu za maziko’’alisema Kamanda Konyo.

 Kamanda Konyo aliongeza kuwa,tayari jeshi lake linamshikilia mtu mmoja akihusishwa na tukio hilo ambaye hata hivyo hakumtaja jina lake kuhofia kuvuruga upelelezi japo alidai kuwepo kwa uhakika wa mtu huyo kujua ukweli wa tukio hilo.

 ‘’Tumemkamata mtu mmoja na tunaendelea kumhoji na tunauhakika kabisa kwamba alihusika na tukio hilo na ni mapema sana kumtaja kwa ajili ya kutovuruga upelelezi wetu tunaye na tunaendelea kumhoji’’alisema Konyo.

 ‘’Lakini kwa kuwa lengo letu lilikuwa kumpata mtoto huyo akiwa hai kwa bahati mbaya sana tumempata akiwa amekufa na tunawaomba watanzania wajitafakari na kuchunguza matendo yetu kama yanampendeza mwenyezi mungu. Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Geita Isaack Timoth mbali na kusikitishwa na kitendo hicho alithibitisha kupatikana kwa mtoto huyo akiwa amekatwa miguu na mikono.

Timoth alisikitishwa na Serikali kutofanya jitihada za kukomesha matukio ya ukatili wanayotendewa walemavu wa ngozi kutokana na matukio hayo kuja kwa kasi. ‘’Kinachotupa shida ni kutokana na sheria mbovu zilizopo mtu mweusi akikamatwa kwa mauaji anahukumiwa lakini Albino anapouawa viungo vyake vinapelekwa hadi kwa mkemia mkuu jambo ambalo linanifanya niamini serikali itakuwa inahusika kutokana na kuwalinda watuhumiwa wa mauaji ya walemavu wa ngozi maana kuna waliokwisha kamatwa na kuachiwa mbali na wananchi kuwatambua na wengine wamehukumiwa kunyongwa lakini adhabu hiyo haijatekelezwa’’alisema Timoth.

 Hata hivyo Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa,katika Wilaya ya Geita kuanzia mwaka 2007-2012 ni walemavu watano walikwishauawa mpaka sasa na tangu kuanzishwa kwa mkoa wa Geita ni mlemavu mmoja ambaye ni mtoto Bahati na idadi yao kufikia sita.

Walemavu hao ni Remmy Juma(2), na Zakaria Juma(7)ambao ni ndugu wakazi wa Buhalahala kata ya kalangalala mjini Geita. Wengine ni Rwegamoyo Kitangili wa Kijiji cha Chigunga,Zawadi Magindu (32)mkazi wa Nyamalulu,Gaspa Elikana wa Nyawilimilwa.

Mbali na waliofariki,uchunguzi pia umebaini kuwa walemavu wa ngozi walioachwa majeruhi na kupewa vilema vya kudumu kuanzia 2007-2011 ni watatu akiwemo Bibiana Mbushi(9)mkazi wa Nyamwilolelwa alikatwa mguu wa kulia na vidole viwili vya mkono wa kulia,Nelick Elias(4) wa Kijiji cha Kaseme aliyenyolewa nywele zake na watu wasiojulikana,Adam Robert(12)mkazi wa Nyaruguguna aliyejeruhiwa mkono wake wa kushoto na kukatwa vidiole vya mkono wa kulia na kutokomea navyo kusikojulikana.



 Mkurugenzi wa Shirika lisiulokuwa la kiserikali linalojishughulisha na kuhudumia watoto yatima,Albino na kutoa msaada wa kisheria la (NELCO),Paulina Alex alidai amepokea kwa masikitiko taarifa za mwili wa mtoto Bahati kupatikana ukiwa umenyofolewa viungo vyake.

 Alex,alisema shirika lake ambalo liliwasaidiwa watoto Albino 80 kupata kiliniki ya magonjwa ymbalimbali huku kati yao 60 wakiwa watoto alilaani Vikali unyama uliofanywa na watu hao na kuitaka jamii kuachana na imani potofu kwamba kiungo cha binadamu kinaweza kuwa tiba ya kuelekea kwenye utajiri.

Kwa upande wake mchungaji Metsoni Asheri wa Kanisa la EAG(T)Tambukaleli mjini Geita aliitaka aliitaka jamii kuachana na imani potofu za kishirikina kwa kutafuta mali na madaraka kwa njia ya kuuawa watu na kwamba laana hiyo ni mbaya isipowadhuru wahusika itadhuru watoto wao.

 ‘’Ninaomba watu wafanye kazi kwa kutumia maarifa na sayansi na kama hawawezi wamuombe mungu atawabariki maana yeye ndiye njia ya kweli na uzima’’alisema Mchungaji Asheri Naye Mchungaji Mathayo Yaya wa kanisa la Heri Wenye Moyo Safi la Mjini Geita mbali na kulaani kitendo hicho aliitaka Serikali kuachana na matamko ya kwenye majukwaa na badala yake ichukuwe hatua kwa watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino) wakiwemo waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi huku akitaja njia rahisi ya kuwabaini ni kutuma makachero nyumbani kwa waganga wa jadi wakijifanya kutafuta utajiri.

‘’Serikali ichukuwe hatua kwa watu hawa kwa vitendo na si kutoa matamko jukwaani pekee na ikibidi itume makachero nyumbani kwa waganga wa jadi wakijifanya wanatafuta njia za kuwa matajiri na pale watakapotakiwa na waganga hao kupeleka kitu chochote kinachoashiria ukiukwaji wa haki za binadamu wanawakamata na ndiyo itakuwa njia pekee ya kukomesha vitendo hiyo’’alisema Yaya.

Tukio la kuibwa kwa mtoto huyo kabla ya mwili wake kupatikana hiyo jana(juzi)ukiwa umenyofolewa viungo vyake,miguu na mikono lilitokea katika kitongoji cha Ilyamchele,kijiji cha Ilelema wilayani Chato mkoani Geita,ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumba ya wazazi wa mtoto Bahati na kuondoka naye kusikojilikana huku wakimjeruhi kwa mapanga mama wa mtoto huyo.

Tukio hilo linalohusishwa na imani za kishirikina lilitokea feb 15 saa 2 usiku na kwa mjibu wa polisi mkoani hapa,Watu wanaodaiwa kufanya unyama huo walikuwa wawili ambao walivamia nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo wakiwa na mapanga na kisha kutoweka naye kusikojulikana baada ya kuwazidi nguvu wazazi wake. Kwa mujibu kamanda wa polisi mkoani Geita,Joseph Konyo,alisema tukio hilo lilitokea saa 2 usiku wakati mama wa mtoto huyo,Ester Jonasi(30)wakati akiwa katika harakati za kuandaa chakula cha usiku.

 Alisema watu hao wakiwa na mapanga baada ya kufika katika familia hiyo,wamteka mama yake na katika kunyang'anyana walilazimika kutumia mapanga kwa kumjeruhi mama wa mtoto huo. Familia hiyo inawatoto watatu wote Albino ambapo wakati mtoto mwingine anatekwa kaka yake alikuwa kwa jirani anacheza na aliporejea nyumbani alikuta tukio limetokea.

 Aidha amesema baba wa mtoto huyo,Bahati Msalaba anashikiliwa na kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo kwani wakati linatokea alikuwa nje anaota moto(Kikome). Hili ni tukio la pili kutokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili ambapo Disemba 27,mwaka jana mtoto Pendo Emanule(4)wa Ndami Misungwi alitekwa na watu wasiojulika na hadi sasa bado hajapatikana wala watekaji wa mtoto huyo hawajakamatwa.

 Mwisho.

Maoni 2 :

  1. unaionaje hiyo ishu

    JibuFuta
  2. oporesheni wa kusaka wauaji alibno iwe endelevu

    JibuFuta