UNYAMA WA KUTISHA GEITA
WANAFUNZI WATATU WAUAWA
KULIPA KISASI CHA WAZAZI WAO
Baba,mama yao na dada hali zao ni mbaya
Na Eliud Dalei,Geita 07/09/2014
WAKATI familia za askari wawili wa kituo cha polisi Bukombe waliouawa
na majambazi usiku wa kuamkia septemba 6 zikiendelea kuomboleza,mauaji mengine
ya kinyama yamefanyika wilayani Geita baada ya watu wasiojulikana kuwachomea
ndani ya nyumba wanafunzi watatu walioteketea na miili yao kubaki mmajivu.
Tukio hilo la kikatiri linalodaiwa kufanywa na mtu aliyekuwa na
ugomvi na familia hiyo, limetokea usiku wa kuamkia septemba 7 saa 8, katika
mtaa wa elimu,kata ya kalangalala Wilayani Geita mkoani Geita.
Akizungumza na gazeti akiwa eneo la tukio ofisa mtendaji wa
kata ya kalangalala mjini Geita Hamad Husein amedai kuwa, tukio hilo linadaiwa
kufanywa na mtu aliyekuwa na ugomvi na familia hiyo uliotokana na mgogoro wa
kiwanja.
Hamad bila kumtaja mtu huyo kwa madai ya kutokuvuruga
ushahidi kabla mhusika huyo hajakamatwa alisema,mtu huyo amefikia hatua hiyo ya
kuichomea ndani ya nyumba familia hiyo na kusababisha vifo vya wanafunzi hao na
wengine kujeruhiwa baada ya kuona haki yake ya kupata eneo hilo ikicheleweshwa.
Husein amewataja wanafunzi walioungulia kwenye nyumba hiyo kisha
kupoteza maisha kuwa ni pamoja na Regnard Robert(9)mwanafunzi wa darasa la nne
katika shule ya msingi ukombozi,Sofia Robert(6)wa darasa la kwanza ukombozi na Remijus Robert(4)mwanafunzi wa darasa la
awali zote zikiwa katika mtaa wa elimu Nyankumbu Geita.
Husein amefafanua kuwa,mbali na miili ya wanafunzi hao
kuteketea kwa moto na miili yao kubaki majibu,hali za wazazi wa watoto hao
akiwemo dada yao mkubwa ni mbaya na wamekimbizwa katika hospitali ya wilaya ya
Geita kwa matibabu zaidi.
Amewataja majeruhi hao kuwa ni pamoja na Robert Remijus(baba
wa familia hiyo),Angelina Gaspar(mama wa familia) pamoja na Scholastika Robert(15)ambaye
dada wa marehemu hao anayesoma kidato
cha pili katika shule ya sekondari mwatulole iliyopo kitongoji cha mwatulole
katika kata ya kalangalala mjini Geita.
Kwa mjibu wa Husein tayari amewasiliana na jeshi la polisi
wilaya ya Geita na wameanza msako wa kumtafuta mtu anayedaiwa kuhusika na tukio
hilo hilo na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha
kumkamata kisha kumfikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Kwa upande wao mwenyekiti wa mtaa huo wa elimu Hassan Mshola
pamoja na mtendaji wa mtaa huo Ally Semfukwe mbali na kulaani vikali mauaji
hayo yaliyotokea kwenye ubalozi wa mchungaji Jonas, wameahidi kufanya kila
iwezekanavyo mtu aliyefanya ukatiri huo anakamatwa mara moja.
Aidha katika tukio hilo mmoja wa watoto wa familia hiyo King
Robert(13)hakuwepo wakati nyumba yao ikiteketezwa kwa moto na kusababisha vifo
hivyo baada ya siku hiyo kulala kwa bibi yake(nyanya)kitongozi cha magema nje
kidogo ya tukio hilo.
Mganga mfawidhi katika hospitali ya wilaya ya Geita Dr Adam
Sijaona amekiri kupokea sehemu ya miili ya wanafunazi hao walioteketea kwa moto
na imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo.
Dr Sijaona amefafanua kuwa,majeruhi mmoja kati ya watatu
ambaye ni Scholastika amepewa rufaa ya kwenda katika hospitali ya rufaa ya Bugando
ya jijini mwanza kutokana na hali yake kuwa mbaya huku wazazi wao wakibaki
katika hospitali hiyo wakiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mjibu wa Dr Sijaona,baba na mama wameungua sehemu za
usoni,mikononi na miguuni huku binti yao aliyehamishiwa Bugando akiungua mwili
mzima.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni