Jumatano, 18 Februari 2015

WALIMU WA VURUGU GEITA WAKALIA KUTI KAVU

 NA ELIUD DALEI,GEITA 17/02/2015

SAKATA la wanafunzi kufunga na kulala kwenye barabara ya Buzilayombo Chato wakishinikiza kuwekewa matuta kupunguza na kuzuia ajali limechukuwa sura mpya baada ya Serikali Wilayani humo kuagiza walimu wakuu kushushwa vyeo vyao.




 Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Omari Manzie Mangochie alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio muda mfupi baada ya vurugu hizo kutulia. Kwa mjibu wa DC Mangochie,walimu wanaotakiwa kushushwa vyeo ni wa shule tatu za msingi Mkapa,Kilimani na Ludete zilizopo katika halmashauri ya mji mdogo wa Katoro,Wilayani hapa,huku walimu wa shule mbili za Sekondari za Nyamigota na Buselesele wakinusurika baada ya kukanusha wanafunzi wao kushiriki kwenye vurugu hizo.

‘’Nimeagiza mamlaka husika kuwashusha vyeo wakuu wote wa shule za msingi Mkapa,Kilimani na Ludete ili liwe fundisho kwa watu wote hasa watumishi wa umma wenye tabia ya kushawishi watu kufanya vurugu kama hizi’’alisema Mangochie na kuongeza ‘’Haiwezekani hata kidogo na haiingii akilini wanafunzi watoto kuchukuwa maamuzi ya namna hii bila kuwepo shinikizo kutoka kwa viongozi wao,hivi inawezekana unamuona mtoto anatoka shuleni na kuingia barabarani na wewe kama mkuu wao unaangalia tu na huchukui hatua…hii haikubariki na lazima kama Serikali tuchukuwe hatua na hatua ya kwanza ni kuwashusha vyeo walimu wakuu wa shule hizi’’alisema.

Mbali na kuwavua madaraka,Mangochie alisema itaundwa kamati maalumu kuchunguza vurugu hizo na atakayebainika kuhusika moja kwa moja zitaangaliwa ni hatua zipi zichukuliwe dhidi yake zikiwemo za kisheria. Katika vurugu hizo ambazo zilizua taharuki kwa zaidi ya saa nane eneo la Standi Mpya Katoro zilitokea(juzi),ikiwa ni siku mbili tangu mwanafunzi Mussa Joseph(9),wa darasa la pili katika shule ya msingi Ludete kugongwa na pikipiki na kufa papo hapo wakati akitoka shule.

Chanzo cha vurugu hizo ni mgomo wa wanafunzi wa shule za msingi Kilimani, Mkapa na Ludete ambapo walilala katikati ya barabara, kushinikiza kuwekewa matuta kutokana na matukio ya ajali ya mara kwa mara hivyo kutishia usalama wao.

 Baadaye vurugu hizo zilipamba moto kutoka kwa wanafunzi na kuingia watu wazima na kuanza kupiga mawe magari yote yaliyokuwa yakipita barabarani na zaidi ya magari saba yaliharibiwa vibaya na watu wakiwemo askari watatu wa kituo kidogo cha polisi Katoro na Wilaya ya Geita kujeruhiwa. Baada ya hali kutulia magari yaliruhusiwa kuondoka hata hivyo hali haikuwa shwari ambapo magari yote yalirudi kituo cha polisi Katoro kwa usalama zaidi.

 MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni