Jumatano, 18 Februari 2015

MLIPUKO WA DHAHABU GEITA WAPOROMOSHA UJAUZITO

 NA ELIUD DALEI,GEITA 15/02/2015


SAKATA la watu sita wakazi wa mtaa wa katoma katika mji wa Geita kupoteza fahamu na wawili kati yao kulazwa kufuatia mshituko walioupata uliotokana na Mlipuko mkubwa katika mgodi wa Dhahabu wa Geita GGM wakati wakilipua miamba ya dhahabu limechukua sura mpya baada ya ujauzito wa mmoja wa wanawake hao Debora Nicholaus(20)kuporomoka akiwa wodini kutokana na mshituko aliokuwa ameupata.




Ujauzito huo wa miezi saba,uliporomoka Feb 13 saa 10 usiku ikiwa ni saa 20 tangu alipofikishwa hospitalini hapo akilalamika tumbo baada ya kutokea kwa mlipuko huo uliozua taharuki mji mzima wa Geita na kusababisha watu kutimua mbio hovyo wakidhani mji umevamiwa na magaidi.

Akizungumza na Gazeti hili kwenye wodi ya wazazi alikolazwa hospitali ya Wilaya ya Geita,Bi,Nicholaus alidai kuwa,siku ya tukio la mlipuko huo Feb 12,2015 majira ya saa 5 asubuhi akiwa nyumbani kwake mtaa wa katoma jirani na eneo la mlipuko alijikuta akidondoka chini na kupoteza fahamu.

 ‘’Nilikuwa nimekaa nikasikia mshindo mkubwa na ndipo nikadondoka chini na kupoteza fahamu nimekuja kuzinduka nipo katika hospitali na baadaye nikiwa hospitalini nilianza kuhisi uchungu wa kujifungua japo ujauzito wangu ulikuwa wa miezi saba haujafikia hatua ya kujifungua mtoto na baadaye majira ya saa 10 usiku wa kuamkia Feb 13 kiumbe kilichokuwa tumboni kilitoka’’

 ‘’Tumeshateseka sana kana kwamba hatuna viongozi wanaoweza kutusemea matatizo yetu,kwani mimi ni wa pili sasa kuharibu kiumbe kilichopo tumboni kwa sababu ya mlipuko kama huo na kuna mwanamke jirani yangu mwaka jana ujauzito wake uliporomoka baada ya kutokea mlipuko kama huo lakini viongozi wetu wapo na hakuna hatua wanazochukuwa’’alilalamika mwanamke huyo huku akibubujikwa na machozi Bibi wa mume wa mwanamke huyo ambaye anamsaidia wodini hapo Cesilia Nicholaus(60)aliitupia lawama Serikali ya Wilaya hiyo kupuuza malalamiko yao ya muda mrefu kutokana na milipuko hiyo jirani na makazi ya watu na kudai kuwa iwapo itaendelea kuwapuuza na kuligeuza suala la kisiasa kama inavyofanya hivi sasa ijiandae kwa maafa makubwa. Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Geita Dk.Adamu Sijaona alithibitisha kuwepo kwa mwanamke huyo hospitalini hapo na kudai kuwa ujauzito huo uliporomoka kufuatia mlipuko huo na kwamba wakati akifikishwa hospitalini hapo alikuwa hajitambui.

 Ofisa Mahusaino wa Mgodi huo Josepha Mangilia hakutaka kuzungumza kitu chochote kuhusiana na sakata hilo na badala yake alimtaka Mwandishi wa habari kwenda kumuona Mwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia kero za watu wa katoma.

Naye mwenyekiti wa kamati hiyo Mathias Bayona iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ya Geita Manzie Mangochie kufuatilia migogoro ya watu wa katoma alisema anafuatilia suala hilo na atatoa taarifa baadaye ya madhara yaliyotokana na mlipuko huo.

Kwa upende wake mwenyekiti wa Mtaa wa Katoma Patrick Faida amesema kamati hiyo iliyoundwa na mkuu wa wilaya ipo kwa ajili ya maslahi yao binafsi kwa alichodai haiwanufaishi watu wa Katoka na badala yake imekuwa ya kisiasa na kwamba inatakiwa kuvunjwa hata kama ni kwa nguvu ya umma.
‘’Hii kamati ya mkuu wa wilaya imetengenezwa kwa ajili ya watu kujipatia ulaji,nimeshamfuata mkuu wa wilaya kumtaka ivunjwe na iundwe nyingine akanijibu sina mamlaka ya kumhoji na kwa sasa nimejipanga kuitisha mkutano wa hadhara na umma ndiyo utaamua cha kufanya juu ya kamati hiyo hata ikibidi umma kuivunja tutafanya hivyo ili kuokoa wananchi wetu’’alisema Faida.

 Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na hata alipopigiwa simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni