Jumatatu, 27 Oktoba 2014

MGAMBO WAFANYA UKATILI WA KUTISHA GEITA

Na Eliud Dalei,Geita 16/09/2014

ASKARI mgambo wawili wa kituo cha polisi cha Nzera kilichopo Tarafa ya Bugando Wilayani Geita Mkoa wa Geita wamefanya unyama wa kutisha baada ya kumshambulia kwa kipigo mwalimu msitaafu kisha kumvunja mbavu zake kabla ya kumtembeza mtaani akiwa uchi wa mnyama.



Mgambo wanaotuhumiwa kufanya unyama huo wanadaiwa kushirikiana na watu wawili ndugu waliotajwa  kwa majina ya  Masalu Mwanangwa na Kona Mwanangwa wote wakazi wa kijiji hicho cha Nzera.

Tukio hilo limetokea Septemba 14 mwaka huu majira saa 3 asubuhi wakati majeruhi Mwalimu Samsoni Mzingwa(58),akielekea shambani kwake.

Akiongea na waandishi wa habari hizi katika hospitali ya Wilaya ya Geita kwenye wodi namba 8 alikolazwa, Mwalimu
Mzingwa alidai kuwa siku ya tukio alishutukia watu wanne wakiwa na mgambo wawili wa kituo hicho cha polis Nzera kisha kumzingira na kuanza kushushia   kipigo kikubwa hali iliyopelekea kupoteza fahamu.

Amesema kana kwamba hiyo haitoshi,walipomaliza kumpiga walimvua nguo zote na kuanza kumtembeza akiwa uchi wa mnyama kabla ya kuokolewa na wananchi wa eneo hilo waliomchukua hadi katika kituo cha afya cha Nzera na baadaye alikimbizwa kwenye hospitali ya wilaya ya Geita kutokana na hali yake kuwa mbaya ambako amelazwa hadi sasa.

Amefafanua kuwa,pamoja na kuwatambua waliomfanyia kitendo hicho hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika ambao wanaendelea kutamba.

 Akifafanua Chanzo cha yeye kupigwa,mwalimu Mzingwa amesema,alikodiswa  shamba mwezi huu kwa ajili ya kulima Maindi na watu aliowataja kwa majina ya Rukasi Bunzali pamoja na Wiliamu Bunzali wote wakiwa ni wanafamilia moja kwa makubaliano ya kuwalipa kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano ambapo aliwalipa pesa zote  na kuanza kulima kwa ajili ya kupanda mazao.

‘’Majuzi wakati nikienda shambani kwangu nilishutukia watu wanne wakiwa na mgambo wawili wa kituo cha polis Nzera kambao walinizingira na kuanza kushushia kipigo kikubwa hadi wakanivunja mbavu huku wakinitembeza uchi wa mnyama lakini wananchi waliniokoa na nilikuja kujikuta nipo hapa hospitalini nimelazwa’’alisema Mzingwa kwa taabu.

Kwa upande wake mtoto wa mzee huyo  Baraka Samsoni amesema baada ya kupata taarifa za kujeruhiwa baba yake alikwenda kujiridhisha na baadaye  alitoa taarifa kwa OCS Nzera lakini hakuna kilichofanyika zaidi ya kutishwa huku akiambiwa asiwafundishe kazi.

Mganga mfawidhi wa Hoaptali ya Wilaya ya Geita Dk Adam Sijaona amekiri mgonjwa huyo kuvunjwa mbavu kutokana na uchunguzi wa awali waliomfanyia.

Mtendaji wa kijiji cha Nzera Henry mapembegamva amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo alilodai kiini chake ni mgogoro wa ardhi.

Kamanada wa polisi Mkoani Geita Josefu Konyo alipopigiwa sm yake ya kiganjani hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.

                                       MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni