Ijumaa, 24 Oktoba 2014

WATOTO WALIOCHOMEWA NDANI WAZIKWA

Na Eliud Dalei,Geita 1109/2014

Miili ya Watoto watatu wa familia moja waliofariki dunia baada kuteketea kwa moto ndani ya nyumba waliyokuwa wamelala katika Mtaa wa Elimu Nyankumbu mjini Geita imezikwa Nyumbani huku simazi,vilio na majonzi vikitawala nyumbani kwa familia hiyo.
 
Miili ya watoto hao,Reginard Robert(9) Mwanafunzi wa darasa la Pili shule ya msingi Nyankumbu,Sophia Robert(6) wa darasa la awali,na Lemijonsi Robert(4)ilizikwa juzi saa 11:30 jioni nyumbani kwao.

Watoto hao waliteketea kwa moto saa 8 usiku wa kuamkia juzi baada ya mtu anayedaiwa kuwa na ugomvi na familia hiyo unaotokana na kugombania eneo la kufyatulia matofari kuiteketeza kwa moto Nyumba hiyo baada ya kuimwagia mafuta ya petroli.

Mazishi hayo yalihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali,dini na wananchi wa maeneo mbalimbali ya mji wa Geita na kuzikwa kwa heshima zote.

Wakati mazishi hayo yakifanyika baba mzazi wa watoto hao,Robert Reginard(49)alionekana kuishiwa nguvu kabisa mbali ya kuwa na majeraha ya kuungua moto kichwani,kilichomuumiza zaidi ni kupotelewa na watoto wake watatu na mmoja akiwa na hali mbaya hospitalini.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Geita,Dk.Adamu Sijaona alisema hali za wazazi wa watoto hao,akiwemo mama yao Angelina Gaspar(38) wanaendelea vizuri isipokuwa binti yao,Scholastika Amos(16) alipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Dk.Sijaona alisema mtoto huyo alikimbizwa Bugando saa 4 asubuhi na gari la kubeba wagonjwa(Ambulance),kutokana na hospitali hiyo ya wilaya kutokuwa na vifaa maalumu vya matibabu kulingana na majeraha ya moto aliyokuwa nayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni