Jumatatu, 27 Oktoba 2014

UHARIBIFU WA MAZINGIRA NUSURA UVURUGE MKUTANO WA CCM GEITA

Na Eliud Dalei,wa goldzoneblog Geita
15/09/2014

Ofisa mazingira wa Halmashauri ya wilaya ya Geita,Hellen Eustace amejikuta kwenye wakati mgumu,baada ya kuzomewa na wananchi wa kijiji cha Nyarugusu wilayani hapa,kwenye mkutano wa Hadhara wa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM),Mkoa wa Geita,Joseph Musukuma kufuatia na uchafuzi wa mazingira wa vyanzo vya maji unaotokana na utitiri wa viwanda vya kuchakata mchanga wa Dhahabu.

 

Eustace alijikuta katika hali hiyo,baada ya kutakiwa na Mwenyekiti Musukuma,kujibu malalamiko ya muda mrefu ya wakazi wa Kijiji hicho yanayotokana na viwanda hivyo kutiririsha maji machafu ya kemikali ya Zebaki ambayo huingia kwenye vyanzo vya maji.

Hatua hiyo ilitokana na Malalamiko yaliyotolewa na wananchi kwenye mkutano huo,ambao walidai kwamba Uchafuzi huo umewafanya kuishi kwa hofu kuhusu Afya zao kutokana na Kijiji hicho kuzungukwa na viwanda vingi ambavyo hutiririsha maji hayo kwenye vyanzo vya maji wanayotumia kunywa,na matumizi mengine ya Nyumbani.

Mmoja wa wananchi hao,Vicenti Mukoma,alidai kuwa wamekuwa wakiishi kwa mashaka kwani kemikali hizo ni hatari kwa Afya za Binadamu na wanayama wengine wakiwemo mifugo na hivyo kumuomba mwenyekiti wa CCM kuchukua hatua juu ya tatizo hilo.

“Mwenyekiti,Nyarugusu inazungukwa na Viwanda vingi sana vya kuchenjua Maludio,na maji yanayotoka kwenye viwanda hivyo yanaingia kwenye vyanzo vya maji tunavyovitegema siku zote,sasa hali hii inatuadhiri Afya zetu”alisema Mukoma.

Baada ya Malalamiko hayo,Mwenyekiti wa CCM aliyekuwa ameambatana na Watumishi wa Halmashauri ya Geita,akiwemo kaimu mganga mkuu,Dk.George Rweyemela,na watumishi wa Nyarugusu,alimtaka Ofisa mazingira kujibu malalamiko hayo mbele ya mamia ya wananchi waliokuwa wamefurika kwenye mkutano huo.

Katika hali ya kushangaza Ofisa mazingira alijikuta akiambulia kuzomewa baada ya kukiri kuwa kweli shughuli za uchimbaji wa madini na uchenjuaji wa dhahabu unaharibu mazingira huku akidai kwamba suala hilo linashughulikiwa na ofisi yake.

“Mwenyekiti ni kweli mazingira yanaharibika,na shughuli zote za uchimbaji hata kule Ng’hwag’alanga mnaharibu mazingira labda tupafunge”alisema hali iliyowafanya wananchi kupinga kauli hiyo na kuanza kumzomea wakimtaka afute kauli yake kwa kuwa kinachoharibu vyanzo vya maji ni Viwanda vya kuchenjua mchanga wa dhahabu na sio machimbo ya wachimbaji wadogo.

Baada ya zomea zomea hiyo,mwenyekiti wa CCM alimtaka kujibu kilichoulizwa na wananchi kuhusu Viwanda hivyo badala ya kuzungumzia machimbo ya wachimbaji wadogo na ndipo alidai kwamba suala hilo linashughulikiwa na ofisi yake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni