Jumatano, 18 Februari 2015

WANAFUNZI WAZUA TAHARUKI GEITA,WATU WAWILI WAJERUHIWA

NA ELIUD DALEI,GEITA16/02/2015

Wanafunzi wa shule tatu za msingi na mbili za Sekondari Wilayani Geita jana walizua tafrani kwa saa zaidi ya nane baada ya kulala na kuandamana katika barabara ya Buzilayombo Chato, eneo la Standi mpya katika mamlaka ya mji mdogo wa Katoro, wakipinga wenzao kugongwa ovyo na magari,akiwemo mwenzao mmoja aliyegongwa na pikipiki Feb14 na kufariki papo hapo. Kufuatia hali hiyo jeshi la polisi Wilaya ya Geita lililazimika kuwatawanya wanafunzi hao kwa kupiga hewani risasi za moto na mabomu ya machozi na kusababisha watu wawili kujeruhiwa sehemu za miguuni na kichwani lakini hawakufua dafu na badala yake wanafunzi hao waliamua kulala katikati ya barabara.




Watoto hao wa shule za msingi Mkapa,Kilimani na Ludete, pamoja na Sekondari za Nyamigota na Buselesele kwa saa kadhaa walitoka madarasani na kwenda kuzuia magari, huku wengine wakiamua kulala barabarani, wakitaka kuwekwa matuta ili kuzuia kugongwa ovyo kwa wenzao.

 Baadhi ya wanafunzi hao wakiwa wameshika mawe, fimbo, kandambili, majani ya miti, walijazana katika eneo la Stand mpya kitongoji cha Kalifonia kata ya Katoro Geita,wakijaribu kuzuia magari kupita hadi yatakapowekwa matuta. Wanafunzi hao wa darasa la kwanza hadi la saba,kidato cha kwanza hadi nne,walizagaa barabarani na wengine wakilala chini, ili kuzuia magari kupita wakipinga wenzao kugongwa,akiwemo Mussa Joseph(9)wa darasa la pili katika shule ya msingi Ludete aliyegongwa na pikipiki Feb 14 na kufa papo hapo.

 Kwa mjibu wa Diwani wa kata ya Katoro,Gervas Daud,akizungumza eneo la tukio alidai kuwa mwanafunzi huyo aligongwa na pikipiki hiyo majira ya saa 5 asubuhi wakati akivuka barabara akitokea shuleni hapo.

Alisema mwanafunzi huyo ambaye amezikwa jana nyumbani kwao katoro alifariki hapohapo kutokana na pikipiki hiyo kuwa kwenye mwendo mkasi na dereva wake hakuweza kusimama kuhofia maisha wake. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kalifonia Elias Muemben zilipo vurugu za wanafunzi hao alidai kuwa,wanafunzi hao wamechukua jukumu la kufunga barabara kufuatia ajali za mara kwa mara eneo hilo ambapo alisema hadi sasa zaidi ya watu watano wamekwishapoteza maisha kwa kugongwa na gari pamoja na pikipiki.

 Alithibitisha kuwepo kwa majeruhi wawili mwanaume mmoja ambaye alijeruhiwa na risasi mguuni na mwanamke mmoja ambaye risasi iliparaza kichwa chake aliodai wamekimbizwa hospitali kwa huduma za kitabibu.

‘’Kuna mwanamke mmoja amepalazwa na risasi kichwani pamoja na mwanaume ambaye ilipita mguuni kwake na wako hospitalini Katoro wakipatiwa matibabu lakini mi naona hawa polisi wasingetumia mabomu ya machozi na risasi za moto na badala yake wangetumia busara maana hali imekuwa mbaya zaidi na wanafunzi wameamua kulala barabarani wakiwa tayari kwa lolote lile na wanadai hawatoki mpaka matuta yawekwe ndiyo maana foleni ya magari imekuwa kubwa kama unavyoiuona’’alisema Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita Joseph Konyo alipotafutwa kupitia simu yake ya Kiganjani namba.0754-027667 ili kuelezea tukio hilo simu yake ilikuwa imezimwa na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni