Jumatano, 18 Februari 2015

OPORESHENI POTEZA CCM KUANZA (KESHO)LEO GEITA

NA ELIUD DALEI,GEITA 16/02/2015

 BARAZA la vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA(BAVICHA),jimbo la Geita linatarajia kuanza ziara maalum kwenye jimbo hilo ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kuikataa katiba inayopendekezwa kwa madai haijakidhi maslahi ya watanzania huku likiahidi kuwafikia wananchi wote wa jimbo hilo hata kama italazimika kutumia usafiri wa mkokoteni unaovutwa na punda kutokana na miundombinu ya barabara kwenye jimbo hilo kuwa mibovu.




 Hayo yamesemwa na makamu mwenyekiti wa BAVICHA jimbo la Geita,Deogratius Shinyanga wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye kikao cha uzinduzi wa oporesheni poteza CCM jimbo la Geita kilichofanyika katika ukumbi wa KG HOTEL ya mjini Geita. Shinyanga alisema,ziara hiyo ambayo itaanza kesho(leo)Feb 17 mwaka huu itajumuisha viongozi mbalimbali wa chama kuanzia jimbo,wilaya ya Geita,Mkoa na Taifa ambapo mwenyekiti wa Baraza hilo Taifa Patrobas Katambi ndiye ataongoza ziara hiyo.

 Akifafanua kuhusu ziara hiyo,Shinyanga alisema,mbali na kujumuisha viongozi wa baraza hilo Taifa pia watakuwepo vijana watatu waliotembea kwa miguu kutoka Geita hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na Rais Jakaya Kikwete na baadaye kuishia mikononi mwa jeshi la Polisi Jijini Dar es salaam.

‘’Hii ziara imelenga kuwafikia wananchi waishio vijijini ambao wamekuwa hawabahatiki kufikiwa na viongozi wa CHADEMA Taifa,ili kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na pia kuikataa katiba inayopendekezwa kwani haijakidhi maslahi ya watanzania’’alisema na kuongeza ‘’Tunajua miundombinu ya jimbo la Geita hasa kwa upande wa barabara si ya kulidhisha na tunawahakikishia tu wananchi wa Geita kwamba ikifika mahali magari yetu yakashindwa kupita na kukwama tutapanda hata mikokoteni ya kuvutwa na punda lakini lazima tuwafikie na kuwafikishia ujumbe tulionao’’.

 Kwa upande wake Katibu wa BAVICHA jimbo la Geita,Gabriel Nyasilu alisema lengo la kuzindua oporesheni poteza CCM Geita ni kuwahamasisha vijana wazilinde,kuzitetea na kuzipigania raslimali zao kwa kuwaondoa viongozi wa CCM kupitia sanduku la kura maana wameshindwa kuwatumikia wananchi na badala yake wamekuwa wakitumikia matumbo yao.

 Aliwataka wananchi wa jimbo la Geita kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwenye mikutano yao ambayo wanaamini itasaidia kuwaamsha vijana kujitambua kwa kushiriki siasa,kugombea,kujiandikisha na kupiga kura.

MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni