NA
VICTOR BARIETY,GEITA 26/06/2015
UPUNGUFU
wa vifaa vya uandikishaji kwenye zoezi la kuandikisha wananchi kwenye daftari
la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR linaloendelea katika halmashauri ya mji wa Geita
limechukuwa sura mpya baada ya baadhi ya vijana kuamua kwenda na chandarua vituoni
huku kinamama wenye watoto na wajawazito wakidai kubaguliwa kwa madai kuwa
kiherehere chao kimesababisha hali walizonazo.
WAKAZI WA GEITA WAKIWA NA VYANDARUA KWENYE
VITUO VYA BVR KAMA WALIVYONASWA NA MPIGAPICHA WETU
VITUO VYA BVR KAMA WALIVYONASWA NA MPIGAPICHA WETU
Hali
hiyo imejitokeza jana(juzi)kwenye baadhi ya vituo vya shule za msingi
Kalangalala na Mtakatifu Aloyce inayomilikiwa na kanisa katoliki jimbo la
Geita.
Mwandishi
wa habari hizi alifika katika kituo cha shule ya msingi Kalangalala na
kushuhudia baadhi ya vijana wakiwa kwenye foleni ya kuandikishwa huku wakiwa
wamebeba chandarua wakijiandaa kulala kwenye kituo hicho iwapo watakosa fursa
ya kujiandikisha kwa siku hiyo ili kuwahi foleni siku inayofuata.
Kwenye
kituo cha shule ya msingi Mtakatifu Aloyce baadhi ya kinamama wenye watoto na
wale wajawazito mbali na kuamka alfajiri lakini hadi kituo kinafungwa majira ya
jioni walikuwa hawajapata fursa hiyo wakidai wanasukumwa na kutishiwa kupigwa
na baadhi ya vijana wakielezwa kuwa kiherehere chao kimepelekea wapate ujauzito
na watoto na kutakiwa kupanga foleni kama wao.
Mmoja
wa akina mama wajawazito Anastazia James(28),mkazi wa mtaa wa Tambukaleli
katika kata hiyo,alidai kuwa pamoja na kuamka alfajiri hadi majira ya jioni
hakupata fursa ya kuandikishwa kutokana na kusukumwa akitakiwa kupanga foleni
kwa madai hawawezi kuruhusu aliyepata ujauzito kwa kupenda apewe fursa hiyo
kama sheria inavyosema.
‘’Nimefika
hapa kuanzia saa 11 alfajiri lakini mpaka sasa sijaandikishwa na nikitaka
kuingia kwenye chumba cha uandikishaji nasukumwa na kutishiwa kupigwa na kwa
hali niliyonayo ya ujauzito siwezi kuhimili kusimama kwa muda mrefu naomba
serikali itusaidie maana kwa hali ilivyo zoezi litamalizika bila sisi
wajawazito kupata fursa’’alisema.
Naye
Jastina Izilael(23),mkazi wa mtaa huo alisema pamoja na kituo hicho kubandikwa
matangazo yanayotoa fursa kwa akina mama wenye watoto,wajawaziti,walemavu na
wajawazito hali imekuwa tofauti maana wao wanabaguliwa.
‘’Nimefika
hapa usiku wa kuamkia leo(juni 15),na nimekuwa kama mtu wa kumi kufika kituoni
lakini pamoja na kukuta mabango yameandikwa wajawazito,walemavu,wazee na sisi
wenye watoto tunapewa fursa ya kujiandikisha hali imekuwa tofauti na kama
unavyoona mpaka sasa kituo kinafungwa sijajiandikisha na siyo mimi tu unaweza
kuona wajawazito na wenye watoto tulivyo wengi kituoni,tunaomba tusaidiwe
jamani’’alilalama.
Mwenyekiti
wa mtaa huo,Mabula Ndoshi akizungumza na kinamama hao nje ya kituo hicho
aliwatoa hofu na kuwaahidi kuwa kadiri siku zinavyokwenda watahakikisha
wanaandikishwa.
Alidai
hali hiyo imetokana na ubovu wa mashine za BVR kuwa mbovu ambapo badala ya
zoezi hilo kuanza asubuhi lilianza mchana kutokana na mashine hizo kuharibika.
‘’Nataka
niwahakikishie tu kwamba,hii vurugu ni kwa sababu mashine ni mbovu ila
tumeongea na mkurugenzi amedai kuanzia kesho mashine zitaongezwa na wote
mtaandikishwa’’alisema Ndoshi.
Kwa
upande wa Mtaa wa Msalala road hali ilikuwa vivyo hivyo ambapo pamoja na mtaa
huo kuwa na watu 3500 wenye sifa za kupiga kura mashine ilikuwa moja na kusababisha
msongamano mkubwa wa watu.
Mwenyekiti
wa mtaa huo,Elineema Mafie aliitupia lawama ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri
ya mji wa Geita kwa kuharibu zoezi hilo kana kwamba walifanya kwa kulazimishwa.
‘’Mtaa
wangu unawatu 3500 wenye sifa za kuandikishwa,na mashine moja inao uwezo wa kuandikisha
watu 140 kwa siku,na zoezi hili limeanza leo(jana) juni 25 na linamalizika
julai 1,kwa hiyo ukifanya hesabu kwa siku hizo watakaoandikishwa ni watau 980
tu na hawa wengine 2,520 inamaana hawatapata fursa ya kuandikishwa’’
‘’Mi
nafikiri serikali kupitia tume ya uchaguzi haikuwa na lengo la kuandikisha watu
ndiyo maana ukiangalia zoezi hili linavyokwenda ni kama wamelazimishwa maana
hata mkurugenzi wa halmashauri ya mji hajashirikisha viongozi wa mitaa husika
na linapelekwa kibubububu tu,labda nyie waandishi mtusaidie’’alisema Mafie.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita Hellen Kahindi
alipotakiwa kuzungumzia changamoto hizo alidai kuwa kadiri siku zinavyokwenda
wanatatua baadhi ya changamoto hizo na kuwahakikishia wananchi kuwa kila mmoja
lazima ataandikishwa.
Kwa
mjibu wa Kahindi,zoezi hilo lililoanza juni 25 kwenye kata za mjini Kalangalala
na Nyankumbu,linatarajiwa kukoma juali 1 mwaka huu ikiwa ni awamu ya tatu na ya
mwisho katika halmashauri hiyo baada ya awamu ya kwanza na ya pili iliyoanza
juni 9 hadi 23,mwaka huu kumalizika kwenye kata za Shiloleli,Bulela,Bung’ hwangoko,Nyanguku,Ihanamilo, Buhalahala
na Mtakuja zilizo nje na mji wa Geita.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni