Jumatano, 22 Julai 2015

MAKAMU WA RAIS BILAL ASISITIZA AMANI YA NCHI

NA VICTOR BARIETY,GEITA

MAKAMU wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal, amewataka waislam na watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanadumisha amani na umoja ulioachwa na waasisi wa taifa hili hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu.



Dkt. Bilal aliyasema hayo jana katika Hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd lililofanyika kwenye  ukumbi wa Shule ya sekondari ya wasichana Nyankumbu iliyopo mjini Geita.


Alisema tangu Karne zilizopita Tanzania  pamekuwa pahala pa amani na utulivu na hivyo kuitaka jamii kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuwafichua watu ambao wanaoharibu amani iliyopo.


Dkt. Bilal alisisitiza  kwamba, amani ni msingi pekee katika taifa kujiletea maendeleo, ambapo alisema  bila amani maendeleo hayawezi kupatikana kwani watu hawatafanya kazi kwa uhuru unao hitajika.



‘’Kiujumla hali ya amani na utulivu imetanda kote katika Mikoa ya Tanzania hali inayopelekea Serikali kupanga na kutekeleza mipango  yake  ya kimaendeleo kwa lengo la kuimarisha uchumi na ustawi wa Wananchi wake sasa naomba kusisitiza amani tuliyo nayo iendelee kudumu pia nawaomba waumini wote mdumishe umoja huu tulionao ili tuweze kusonga mbele,alisema dkt. Bilal.


Mbali na kutoa wito huo Dk. Bilal alilaani mauaji yaliyotokea  nchini Burundi na kuwataka viongozi wote duniani kukaa na kujadili namna ya kurejesha amani hiyo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatuma Mwassa alimpongeza Dkt. Bilal kwa uongozi wake mzuri katika kipindi cha awamu ya nne,  chini ya Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete kwani wamefanya mengi nchini likiwemo suala la uhuru wa watu kujieleza na kutoa maoni yao.


“Nakupongeza sana kwa uongozi wako  katika kipindi cha awamu ya nne chini ya rais wetu Dkt. Jakaya Kikwete, mmefanya mengi hasa katika Mkoa wetu wa Geita na Tanzania kwa ujumla na kwa niaba ya wananchi wa Geita tunawashukuru kutupatia mgombea urais kutoka Mkoa wetu wa Geita Mh. John Magufuli,’’alisema Mwassa.

Naye katibu Mkuu wa Baraza Kuu  la Waislamu Tanzania (BAKWATA),  Sheikh Suleiman  Lolila aliwataka waislam na watanzania kwa ujumla wenye vigezo vya kupiga kura wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura pindi zoezi hilo litakapowadia Oktoba 25 mwaka huu.


MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni