NA VICTOR BARIETY,GEITA
WAUGUZI na wahudumu wa afya katika hospitali ya wilaya ya geita wamemkataa mganga mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Noel Makuza kwa madai kuwa amekuwa akitumia ubabe pamoja na lugha chafu kwa wafanyakazi hao.
Wakitoa malalamiko hayo jana mbele ya Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa afya (TUGHE) Taifa Archie Mntambo, watumishi hao wa afya walisema kuwa Dkt. Makuza amekuwa kikwazo kwao, mbali na kutoa lugha chafu pia ameshindwa kuidhinisha fedha za malipo yao mbalimbali, yakiwemo malimbikizo ya fedha za likizo na malipo kwa saa za ziada kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa TUGHE tawi la hospitali ya wilaya, Mary Muntu alisema kuwa kiongozi huyo wa hospitali hana sifa za kuongoza watumishi wanaohudumia wagonjwa katika hospitali hiyo kutokana na kukosa hekima na busara za kiuongozi katika kuongoza watu walio chini yake.
Muntu alisema kuwa kutokana na tabia yake ya ubabe na lugha chafu kwa watumishi wenzake hali hiyo inasababisha kudhorota kwa huduma ya afya siku hadi siku.
“Hakuna maelewano mazuri baina ya mganga mkuu na wafanyakazi wengine..uongozi wa hospitali HMT unapopeleka malalamiko kwa uongozi uliopo chini yake CHCMT hakuna majibu ya kulidhisha ambayo yanatolewa kutokana na kutumia nafasi yake hiyo kwa ubabe”alisema Muntu.
“Nilibambikizwa nikakamatwa na rushwa ya sh. 1000 iliyotengenezwa na Dkt. Makuza kwa sababu nafuatilia maslahi ya watumishi wenzangu..lakini kwa kuwa siku zote haki ya mtu haipotei nilishinda hiyo kesi mahakamani baada ya kukaa zaidi ya mwaka mmoja nikiwa nje ya kazi nimesimamishwa…mbali na hilo pia anatabia ya ubabe na lugha chafu kwa watumishi,amefuja fedha za watumishi za likizo, malipo ya saa za ziada kazini’’aliongeza Muntu.
Thabitha Shiduki Muuguzi wa hospitali hiyo alisema tangu aajiliwe hospitalini hapo, hajawahi kulipwa fedha zake za likizo licha ya fomu zake kuzipeleka kwa DMO lakini zimekuwa zikitupiliwa mbali pasipo kushughulikiwa.
“Kuna tatizo kubwa hapa sijawahi kulipwa fedha yangu ya likizo, pamoja na hayo mimi binafsi sina mahusiano mazuri na mganga mkuu kutokana na lugha zake chafu hana ushirikiano hata kidogo ofisi yake naiona kama kituo cha polisi,alisema Shiduki.
Kutokana na hilo, wauguzi pamoja na wahudumu wa afya, kwa pamoja walimuomba Mwenyekiti huyo wa tughe taifa Archie Mntambo awasaidie kumuondoa DMO huyo kwasababu amekuwa ni kero hospitalini hapo.
Naye Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Adamu Sijaona alikiri kuwepo kwa changamoto hizo hospitalini hapo na kwamba malalamiko ya watumishi wenzake amekuwa akiyafikisha panapohusika.
‘’Stahiki za watumishi zipo kisheria, kuna likizo, mavazi ya wauguzi, matibabu, malipo ya ziada kuna kupandishwa vyeo na nyumba za madaktari..kakweli kuna tatizo kwa namna moja ama nyingine,’’alisema Dkt. Sijaona.
Kufuatia hali hiyo Mwenyekiti huyo wa TUGHE taifa Archie Mntambo alimwagiza afisa utumishi wa halmashauri ya wilaya ya Geita kumpatia uhamisho mganga huyo ili kuondoa msuguano uliopo.
“Nawaomba halmashauri mlitafakari hili na ikiwezekana mpatieni uhamisho DMO..ili sasa muondoe kero zilizopo hapa kwasababu akiendelea kuwepo ufanisi wa kazi utapungua na matatizo makubwa yanaweza kutokea…waathirika wakubwa wa mgogoro huu ni wananchi na si watumishi,’’alisema Mntambo.
Hata hivyo Mganga Mkuu Dkt. Noel Makuza hakuweza kutokea katika kikao hicho cha watumishi wa afya wa hospitali hiyo kwasababu ambazo hazikuweza kujulikana mara moja na alipopigiwa simu yake ya kiganjani hakupokea na wala hakujibu ujumbe wa maandishi aliotumiwa
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni