GEITA WAIWEKA KAMATI KUU YA CHADEMA TAIFA,MSALABANI!
BAADHI ya wapenzi
na wanachama wa chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA),Mkoa wa Geita wenye
mapenzi mema na chama hicho wameishauri kamati kuu ya chama hicho Taifa ambayo
imepewa jukumu la kuthibitisha majina ya makatibu wa jimbo,wilaya na mkoa
kufanya maamuzi magumu kwa kuwaondoa kwenye nafasi hizo baadhi ya wateule wa
nafasi hizo wasio na sifa.
Pia
wanachama hao wameuomba uongozi wa chama hicho Taifa kuwaondoa kwenye nafasi
zao baadhi ya wagombea waliochaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali kwenye chama
hicho hasa wale waliopita kwa harufu ya rushwa kinyume cha katiba ya chama
chao.
Wanachama
hao wamefikia hatua hiyo baada ya kugundua kuwa wateule wa nafasi hiyo ngazi ya
wilaya na mkoa wa Geita walipitishwa kwenye nafasi hiyo kimizengwe mbali na
kutokuwa na sifa za kuweza kuimudu.
Wateule
kwenye nafasi hizo wanaodaiwa kupitishwa kimizengwe,kwa upande wa katibu wa wilaya
ya Geita ni Rogers Luhega ambaye awali alikuwa katibu wa jimbo la Geita kabla
ya nafasi yake kuchukuliwa na Mutta Robert ambaye kitaaluma ni mwanasheria,huku
nafasi ya katibu wa mkoa wa Geita ikichukuliwa na Sudi Tanyagara.
Sababu za
wanachama hao kuitahadharisha kamati kuu kufanya maamuzi magumu ili kukinusuru
chama hicho kwa kuwaondoa kwenye nafasi hizo wateule hao ni pamoja na mienendo
yao inayotia shaka ndani ya chama
inayoashiria kukivuruga chama hicho wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa
serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Pamoja na
mambo mengine,wanachama hao wameonyeshwa kukerwa na kauli aliyoitoa Katibu
mteule wa chama hicho Mkoa wa Geita Sudi Tanyagara muda mfupi baada ya
kutangazwa mshindi kauli waliyodai ikifumbiwa macho inaweza kukisambaratisha
chama hicho.
Tanyagara huku
akirekodiwa na mitambo ya JAMUHURI,akigeuka kituko ukumbini baada ya kutangaza
hadharani kuwa katika uongozi wake hatafuata katiba ya chama hicho kutatua
migogoro mbalimbali jambo lililotafsiliwa kuwa iwapo kiongozi huyo atathibitishwa
rasmi na kamati kuu,uongozi wake utakuwa wa kidikiteta usiojali utu wa
mwanadamu na misingi ya kidemokrasia.
Chanzo cha
katibu huyo kutoa kauli hiyo,ni baaada ya baadhi ya wajumbe wa mkutano huo
kupendekeza wagombea wawili kati ya watano Neema Chozaile na Julius Marco
warudiwe kupigiwa kura kwenye nafasi ya uenyekiti BAWACHA mkoa wa Geita kwa
kuwa mshindi katika nafasi hiyo Chozaile hakufikisha 50 asilimia kama katiba ya
chama hicho inavyosema.
‘’Mheshimiwa
mwenyekiti katiba ya chadema toleo la 2006 ibara ya 6.3.1(C) inasema majina ya
wagombea wote wenye sifa zinazotakiwa watapigiwa kura ya siri na kikao
kinachohusika na mshindi atapatikana kwa wingi wa kura usiopungua 50 asilimia
ya wapiga kura halali waliohudhuria kikao cha uchaguzi na kwa kuwa kwenye
nafasi ya uenyekiti BAVICHA mshindi(Chozaile)hajafikisha hiyo asilimia tunaomba
warudie kupigiwa kura’’alisikika mjumbe mmoja akishauri.
Hata hivyo
katika hali isiyotarajiwa Katibu mteule wa Chadema Mkoa wa Geita Tanyagara
alisimama na kupinga mapendekezo hayo kwa kile alichodai katiba haiko juu ya
wadhifa alionao na kumtaka mwenyekiti afunge kikao watu warudi majumbani mwao.
‘’Nasema
hivi hakuna cha katiba inasemaje,mimi ndiyo katibu wa mkoa wa Geita hapa
uchaguzi haurudiwi,mimi kama katibu nimesema na katika uongozi wangu
sintokubali katiba ya chama itawale maamuzi yangu mwenyekiti naomba ugunge
kikao na kama kuna mtu hajaridhika atakata rufaa kwangu’’alifoka Tanyagara na
kusababisha ukumbi mzima kulipuka ukiashiria kupinga udikteta wake.
Kufuatia
hali hiyo,mwenyekiti mteule wa Chadema Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo akionyesha
kukerwa na kauli hiyo alisimama akitaka kuwatuliza wajumbe lakini msimamizi wa
uchaguzi huo Cosmas Makune alimsihi akae chini na msimamizi aliamua kufuata
katiba kwa kurudia uchaguzi wa nafasi hiyo na Chozaile kuibuka tena mshindi.
Kwa mjibu wa
wapenzi na wanachama wa chama hicho ambao wamekuwa wakifuatilia nyendo za
kiongozi huyo walidai kuwa,hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa katibu huyo kufanya
maamuzi kidikiteta,katika uchaguzi wa jimbo la Busanda Geita Tanyagara akiwa
msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika Agost 10 mwaka huu kwenye nafasi ya
uenyekiti alimtangaza mshindi wa nafasi hiyo pamoja na kura kuzidi wapiga kura.
Wagombea
kwenye nafasi hiyo walikuwa watatu,na wapiga kura 109,ambapo George Kwacha kura
46,Julius Marco 44 na Joseph Butondo 21 ambapo idadi ya wapiga kura inakuwa 111
lakini alimtangaza Kwacha kuwa mshindi badala ya uchaguzi kurudiwa.
Vivyo hivyo
kwenye nafasi ya ukatibu wa jimbo hilo ambapo Vedastus Mtasigwa alipata kura
48,Deogratius Sangalali 60 na kura 1 iliharibika lakini aligoma kumtangaza
mshindi kwa kuwa aliyeshindwa ni rafiki yake wa karibu.
Hali hiyo
imezidi kuwashitua baadhi ya wanachama wa chama cha hicho na kuiomba kamati kuu
ya chama hicho Taifa kutomthibitisha katika nafasi hiyo kwa kuwa ameonekana
hana sifa za kiuongozi.
Kwa upande
wa Luhega,wanachama hao wamedai hana sifa za kukiondoa chama hicho kilipo
kutokana na walichodai hata alipokuwa katibu wa jimbo la Geita alishindwa
kuwaunganisha wanachama na badala yake alizalisha makundi ambayo yalikwishaanza
kukitafuna chama hicho.
Pia walidai
hata nafasi yake aliipata kwa kubebwa na msimamizi wa uchaguzi huo Njugu
Tungaraza aliyemtangaza kuwa katibu mpya
wa wilaya ya Geita mbali na wajumbe wa mkutano huo kumpigia kura 9 za
hapana kati ya kura 16 katika uchaguzi
uliofanyika Agost 29 mwaka huu.
Kituko hicho
cha uvunjaji wa katiba na miongozo ya uchaguzi kilitokea ndani ya ukumbi wa
Hotel ya kisabo mjini Geita katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa mabaraza na viongozi
wa wilaya wa chama hicho.
Wagombea
katika nafasi hiyo walikuwa wawili Mapesi Maagi na Rogers Luhega na katika kile
kinachoonyesha zoezi hilo lilitawaliwa na mianya ya rushwa msimamizi wa
uchaguzi huo Njugu Tungaraza aliondoa jina la Maagi dakika za majeruhi ukumbini
hapo ili Luhega apite bila kupingwa.
Hali hiyo
ilipelekea wajumbe wa mkutano huo kucharuka wakihoji sababu za Maagi kuenguliwa
bila majibu ya kuridhisha zaidi ya kuambulia vitisho kutoka kwa Tungaraza.
Hata hivyo
katika kile kilichoonyesha hasira za wajumbe hao hata baada ya kuweka jina moja
la Luhega katika kinyang’anyiro hicho ili lipigiwe kura za ndiyo na hapana kura
zilizopigwa nyingi zilikuwa za hapana lakini haikumzuia msimamizi kumtangaza
Luhega kuwa mshindi wa nafasi hiyo.
Kura
zilizopigwa zilikuwa 16 na kati ya hizo Luhega ambaye hata hivyo hakuwepo
katika uchaguzi huo alipigiwa kura 9 za hapana na 7 za ndiyo lakini msimamizi
aliamua kumtangaza kama mshindi huku akijitetea kuwa,amefanya hivyo kwa lengo
la kupunguza makundi ndani ya chama.
‘’Inakuwa
siyo vizuri mtu aliyekuwa kwenye system leo aondolewe hivi hivi...huyu alikuwa
katibu wa chama jimbo la Geita na ameshindwa kwenye nafasi hiyo nah ii nayo
mnataka mmuondowe..ndiyo maana nimeamua kuondoa jina la Maagi ili apite bila
kupingwa na kwa kuwa mmempigia kura za hapana mimi namtangaza mshindi kwenye
nafasi hiyo na ambaye hajaridhika anaweza kukata rufaa’’alisikika Tungaraza
akitamba na kuwaacha wajumbe wa mkutano huo midomo wazi wasijuwe la kufanya.
Aug 11
mwaka huu kabla ya kupewa nafasi hiyo kwa kura za hapana Kamati kuu ya Chadema ilimvua Luhega wadhifa wa
ukatibu wa jimbo kwa tuhuma za kutumia madaraka yake vibaya,ikiwa ni siku
moja baada ya yeye na kamati yake tendaji ya jimbo kumvua uanachama
Diwani wa viti maalumu(Kagu), Maliselina Simbasana ambapo piqa amekuwa akituhumiwa kumuunga mkono mbunge wa
Kigoma kaskazini Zitto Kabwe pamoja na kwamba amekuwa akikana tuhuma hizo.
Kufuatia
hali hiyo, Katibu wa wazee wa chama hicho Amos Nyanda alipewa na uongozi wa kanda jukumu la kuratibu na kusimamia
chaguzi zote baada ya viongozi wa jimbo akiwemo Luhega kukosa sifa ya kufanya
hivyo.
Hii si
mara ya kwanza kwa Luhega kutumia madaraka yake vibaya ambayo kwa kiasi kikubwa
yamekiathiri chama hicho.
Julai 27
aliamua kuufuta uongozi wa kata ya kalangalala na mabaraza yote ya chama hicho
kwenye kata hiyo.
Uchaguzi huo
wa Mabaraza ulifanyika baadaye kwa agizo kutoka kamati kuu ya chadema Taifa chini
ya uratibu wa Nyanda ulifanyika Aug 14 ukisimamiwa na viongozi wa kanda ya ziwa
magharibi.
Kituko kingine alichofanya msimamizi huyo,pia kwenye
nafasi ya mkutano mkuu wa Taifa wagombea wawili kati ya 6 waliokuwa wakiwania
nafasi hiyo waligongana kura lakini msimamizi aliamuru mwenyekiti wa kikao
hicho aliyemteuwa yeye(msimamizi),kupiga kura ya turufu kwa mmoja wa wagombea
ili kumpa ushindi kinyume cha taratibu za uchaguzi.
Aliyepigiwa
kura ya turufu na mwenyekiti wa kikao hicho na kupatiwa ushindi wa upendeleo ni
Aloyce Shigela(Mtafiti wa nyaraka na utafiti wa Chadema Mkoa wa Geita)cheo
ambacho pia hakiko kikatiba aliyekuwa
akichuana na Daud Ntinonu.
Wengine
walioenguliwa kimizengwe ni Sophia Ludandali aliyekuwa ameomba nafasi ya
uenyekiti wazee wilaya ya Geita na badala yake nafasi hiyo alipewa Amosi Nyanda
kwa kubebwa aliyekuwa ameomba ukatibu wazee Wilaya.
Pia Beatrice
Maganga aliyekuwa ameomba ukatibu wa wanawake Wilaya naye alienguliwa kwenye
kinyang’anyiro hicho dakika za majeruhi na nafasi hiyo kuachwa wazi bila sababu
za msingi lengo likielezwa ni kudhoofisha kambi inayomuunga mkono mwenyekiti wa
chadema Taifa Freeman Mbowe na kuimalisha kambi ya Luhega ambayo imekuwa
ikiunga mkono harakati za Zitto Kabwe.
Tayari
wagombea wote ambao wamefanyiwa mizengwe kwenye nafasi walizoomba wamekata
rufaa ngazi husika wakipinga msimamizi huyo kuendesha zoezi hilo kibabe bila
kujua kwa kufanya hivyo ni kukiathiri chama chao.
Pia
Husna
Amri ambaye ni mratibu wa BAWACHA Mkoa wa Geita na ambaye amefanikiwa
kutetea
nafasi hiyo,anatuhumiwa kupita kata 11 kati ya 22 za wilaya ya Chato
Mkoa wa
Geita akiwahadaa akina mama kumchagua kwa madai kuwa amepewa
fungu(pesa)na Josephine Mushumbusi kwa ajili ya kuwawezesha wanawake
kwenye vikundi vyao vya ujasiliamali.
Mshumbusi ni
mke wa katibu mkuu wa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA),Dr Wilbrod
Slaa na kuwaahidi watakapomchagua atawagawia pesa hizo kwa ajili ya kujikwamua
kiuchumi.
Kwa mjibu wa
Husna vikundi hivyo vilipaswa kuundwa na wanawake wasiopungua 30 hali ambayo
kwa sasa imejenga chuki baina ya wanawake hao na Mshumbusi baada ya kubaini
ilikuwa janja nyani ya kujinadi ili kujipatia kura kupitia mgongo wa mke huyo
wa Dr Slaa.
Baadhi ya
kata alizohadaa wanawake hao ni pamoja na
Bwanga,Buziku,Bukome,Makurugusi,Butengolumasa,Buseresere na Bwela.
Baadhi ya
viongozi wa kata hizo akiwemo Josephat Manyenye kutoka kata ya Bwela anakiri
Amri kupita kwenye kata hizo na kuwahadaa baadhi ya kina mama na yeye baada ya
kumfuma akifanya hivyo alimtimua kwenye kata yake huku akimuonya kutokanyaga
tena maeneo hayo kabla na baada ya uchaguzi huo uliomweka madarakani.
Kwa sasa Husna
ndiye mratibu wa BAWACHA wa chama hicho Mkoa wa Geita baada ya kufanikiwa
kuwahadaa kinamama hao na alichaguliwa Agosti 30 mwaka huu na wenyeviti wa BAWACHA kutoka kwenye majimbo
yote ya Mkoa wa Geita.
Mshumbusi
alipotafutwa kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo iwapo alimtuma
kufanya hivyo simu yake ilikuwa haipatikani na gazeti hili linaendelea
kumtafuta na mahojiano yake yatapewa uzito wa kipekee kwenye gazeti hili ili
jamii wakiwemo kinamama hao wafahamu kile alichokisema.
Hata hivyo Amri
alipopigiwa simu na gazeti hili Septemba 5 mwaka huu saa 13:26 na kuongea kwa
sekunde 00:00:57 badala ya kutoa ushirikiano aliporomosha matusi ya nguoni kwa
mwandishi wa habari hizi na mengine hayawezi kuandikika.
‘’We
mse.......nini.......nitolee upumbavu wako hapa’’alifoka Amri kisha kukata
simu.
Kada
mwingine wa chadema anayedaiwa kukivuruga chama hicho ni Neema Chozaile,ambaye
ni mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Geita aliyechaguliwa hivi karibuni katika
uchaguzi uliofanyika Agost 30 mwaka huu.
Pamoja na
mambo mengine,Chozaile anatuhumiwa kama kinara wa vurugu zilizotokea kwenye
uchaguzi wa viongozi wa chama na
mabaraza ya(CHADEMA)katika kata ya Kalangalala mjini Geita zilizopelekea
mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukaleli kupitia chama hicho kujeruhiwa vibaya mdomoni
na mgongoni.
Tukio
hilo lilitokea Agost 14 mwaka huu majira ya saa 6:46 mchana muda mfupi baada ya
wasimamizi wa uchaguzi huo kutoka kanda ya ziwa magharibi kuwasili eneo la
uchaguzi huo amabo awali ulitakiwa kufanyikia kwenye ukumbi wa ofisi ya
serikali ya mtaa wa Mkoani inayoongozwa na Chadema.
Mapema
asubuhi kabla ya ugeni huo kuwasili eneo hilo hali ya usalama na utulivu
ilikuwa imetanda huku wananchama wa chama hicho wakiwa wamekaa makundi
wakibadilishana mawazo na kila mmoja akiwa na shauku ya uchaguzi huo.
Hata hivyo
katika hali isiyokuwa ya kawaida katibu wa mwenyekiti wa mtaa huo wa
Mkoani,Peter Donald(CHADEMA)alifika eneo hilo kisha kufunga ukumbi uliokuwa
umeandaliwa kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi akidai kufanya hivyo kutokana na
maagizo aliyopewa kutoka juu kisha kuondoka eneo hilo akiwaacha wanachama wa
chama hicho wakiwa wameduwaa.
Majira ya
saa 6:23 wasimamizi kutoka kanda waliwasili eneo hilo wakiwa na gari namba T
156 CDA aina ya Ranger Ford na kuelezwa kuwa ukumbi wa chama chao uliokuwa
umeandaliwa kwa ajili ya kikao ulikuwa umefungwa kwa maelekezo ya aliyekuwa
katibu wa jimbo hilo kabla ya kuvuliwa madaraka Rogers Luhega akishirikiana na
mwenyekiti wa mtaa huo Peter Donald ambaye pia ni diwani ya kata hiyo kupitia
chama chao.
Wakati
ugeni huo ukipata maelezo hayo lilitokea kundi la wanachama wa chama hicho
linalomuunga mkono Luhega kisha kuvuruga maongezi hayo na kuanza kuporomosha
matusi ya nguoni kwa wasimamizi hao kutoka kanda na kwa baadhi ya viongozi wa
chama hicho akiwemo Daud Ntinonu aliyedhalilishwa kwa kila aina ya matusi
lakini hakujibu lolote.
Kundi
hilo lililokuwa likiongozwa na baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo Neema
Stephen Chozaile(Mratibu Bavicha Mkoa wa Geita),Elikana Gidion(Katibu mwenezi
tawi la Nyanza),Peter Mazura(bodigadi wa kujitegemea wa Luhega),Sospiter
Sweya(Mwenyekiti tawi la mwatulole)
Tom
Revons(Katibu tawi shilabela),Fikiri Charles Toi(Mwenyekiti kata ya kalangalala
aliyejihudhuru)na Albert Machumu pamoja na mambo mengine lilijiapiza kuwa liko
tayari kupoteza maisha lakini si kushuhudia uchaguzi huo unafanyika.
Wakati
hayo yakiendelea wasimamizi wa uchaguzi huo walikuwa kimya wasijue la kufanya
na baada ya muda kundi hilo lilibeba mawe na kuanza kuwashambulia wenzao na
moja likatua mdomoni na mgongoni kwa mwenyekiti wa mtaa wa Tambukaleli Mabula
Ndoshi aliyejeruhiwa vibaya.
Kufuatia
hali hiyo baadhi ya wanachama walitimua mbiyo huku dereva wa gari lililokuwa
limebeba wasimamizi hao akitumia uzoefu wake kwa kuwabeba viongozi hao kisha
kuliondosha kwa kasi gari hilo ambalo liliokolewa na Redbrigade wa chama hicho
waliofika eneo hilo mara moja kisha kuwadhibiti kundi lililoleta vurugu ambalo
nalo lilitimua mbio kukwepa mkong’oto kutoka kwa vijana hao wa ulinzi wa
chadema.
Vurugu
hizo zilitulia majira ya saa 7:40 na msamalia mmoja wa eneo hilo alitoa ukumbi
na uchaguzi ukaendelea kwa amani ambapo hata hivyo baada ya kura kupigwa
uongozi wote wa kata hiyo chama na mabaraza uliokuwa umefutwa kimizengwe na
aliyekuwa katibu wa chama hicho jimbo la Geita,Luhega ulichaguliwa kwa mara
nyingine tena.
Siku moja kabla
ya uchaguzi huo aliyekuwa katibu wa chama cha demokrasia na
maendeleo(CHADEMA),jimbo la Geita,kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na kamati kuu
ya Chadema Taifa Luhega na anayedaiwa
kuwa kambi ya mbunge wa kigoma kaskazini Zitto Kabwe aliapa kuzuia huo uchaguzi
wa kata na wa jimbo usifanyike mbali na maagizo hayo kutoka kamati kuu Taifa ya
Chadema iliyoagiza uchaguzi huo ufanyike ndani ya wiki hii tambo ambazo hata
hivyo ziligonga ukuta na chaguzi zote hizo zikafanyika.
Kabla ya kufanyika kwa chaguzi hizo baadhi ya wanachama wa cha Demokrasia na Maendeleo
Chadema wa kata ya Kalangalala mjini Geita walirushiana ngumi wakituhumiana
kuchukua rushwa kuvuruga uchaguzi wa kata hiyo sakata lililotokea saa 1 jioni kwenye Hoteli ya
Wandela Mjini Geita,baada ya kundi la Luhega wakiwemo baadhi ya wagombea wa
nafasi mbalimbali wa kata na jimbo kukutwa likipanga njama chafu za kuhujumu
uchaguzi huo.
Mwisho.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni